• Author
  Posts
 • #815

  Mabula Emmanuel
  Keymaster

  Elimu Ya Masoko
  Na Deodat Bernard

  Katika makala yaliyopita tulijifunza maana halisi ya soko, matakwa na mahitaji ya wateja yanayohitaji kutimizwa na bidhaa au huduma zinazotolewa na biashara. Makala haya yanajikita katika kukupa mbinu za kuuza na kukuza mauzo katika biashara yako. Kwa kawaida, lengo kuu la biashara ni kutoa huduma na kupata faida. Faida ya bishara inategemea ukubwa wa soko la bidhaa au huduma za biashara yako. Masoko ni kila kitu kinachofanyika kwa lengo la kushawishi wateja watarajiwa waweze kuona thamani na wailipie kwa ajili ya kupata bidhaa au huduma zinazotolewa na biashara. Sehemu ya kiasi cha fedha kitakacholipwa na mteja katika kupata bidhaa au huduma, ndicho kinachokuwa faida katika biashara.

  Hebu tutazame mbinu mbalimbali ambazo mmliki wa biashara anaweza kutumia kwa ajili ya kuimarisha na kukuza mauzo ya biashara yake.
  Fanya masoko kuwa ni kipaumbele cha kwanza Sababu kubwa itakayomfanya mteja achague na kununua bidhaa au huduma zako ni ushawishi anaoupata kutokana na jinsi unavyoitangaza na kuuza katika biashara yako. Inapasa matangazo ya biashara yako yaanze mapema kabisa wakati unawaza kuzalisha bidhaa kwa ajili ya wateja wako. Unapotengeneza bidhaa, ni lazima uzingatie mahitaji muhimu ya wateja na kuyatimiza. Mahitaji haya yanaweza yakawa ni ukubwa, rangi, mwonekano, urahisi wa kubeba, urahisi wa matumizi na mahitaji mengine, kulingana na aina ya bidhaa husika. Hakikisha mahitaji haya yanatimizwa kwani yatawashawishi wateja watarajiwa kununua bidhaa pindi tu zitakapowekwa sokoni. Jambo jingine la kuzingatia ni bei utakayouzia bidhaa au huduma zako. Hapa unatakiwa kuchagua bei itakayokuwezesha kupata faida. Vilevile unapaswa kupanga bei ambayo wateja wataweza kuilipia na kujihisi bidhaa au huduma waliyoinunua ina thamani kubwa kuliko kiasi cha pesa walichotoa. Linganisha bei ya bidhaa zako na ile ya washindani wako, na pia aina ya wateja unaowalenga katika biashara yako. Pata maoni ya wateja wako kuhusu bidhaa au huduma wanayotaka na bei ambayo wataweza kulipia. Baada ya bidhaa au huduma kuwa tayari, kinachotakiwa ni uhamasishaji kufanyika kwa jitihada kubwa. Wasiliana na wateja walengwa na kuwapa taarifa ya ujio wa bidhaa au huduma mpya sokoni. Aidha waarifu kuhusu faida zake, na ni kwa nini waanze kutumia

  bidhaa au huduma hiyo.
  Matokeo ya matangazo hayo yanakuwa ni mauzo, hususan wateja watakapoona thamani ya bidhaa au huduma ni kubwa kuliko bei wanayolipia. Matangazo kwa ajili ya biashara yako hayatakiwa kukoma. Yaendelee kila wakati ili kuwakumbusha, kuwataarifu na kuwashawishi wateja waendelee kuamini bidhaa au huduma zinazotolewa na biashara yako ndizo bora zaidi.
  Fanya Zaidi ya Matangazo
  Matangazo ya biashara ni sehemu tu ya masoko. Ili kufanikiwa katika biashara, ni lazima kufanya zaidi ya matangazo ya biashara. Zingatia hatua tatu muhimu za mwanzo ili matangazo yawe na matokeo mazuri katika mauzo. Angalia ubora wa matangazo yako ya biashara jinsi yanavyoweza kuleta ushawishi na kuwavutia wateja, ili hata wale ambao hawakuwa na mawazo ya kutumia bidhaa au huduma za biashara yako waweze kuwa na hitaji hilo. Nasema hili kwa sababu kuna baadhi ya wateja wanalinganisha ubora wa matangazo na bidhaa au huduma inayouzwa.
  Wafahamu Vizuri Aina ya Wateja Unaowalenga
  Kama nilivokwisha kueleza katika makala yaliyopita, ni lazima kufanya utafiti wa kutosha kuhusu wateja u n a o w a l e n g a . Fahamu mahitaji na uwezo wa kila aina ya wateja wanaolipia bidhaa. I k i w e z e k a n a unapofanya utafiti huo, waweke katika makundi ili uweze kufahamu tabia zao za ununuzi, jinsi wanavyotofautiana na ni nini hitaji la kila mmoja. Inabidi ujue wananunua wapi bidhaa, wanapenda nini na ni kitu gani wangependa kukipata ila wanakikosa, ili na wewe uweze kuwatimizia. Maswali yafuatayo yanaweza kukusaidia wakati wa utafiti wa kujua mahitaji ya wateja wako watarajiwa:
  • Kwa nini wananunua bidhaa au huduma fulani?
  • Bidhaa au huduma zinawafikiaje?
  • Wananunua mara ngapi, na ni kipindi gani wananunua?
  Zingatia Ushauri na Mawazo ya Watu Wengine
  Mara nyingi imekuwa ni kawaida kwa wamiliki wa biashara kujiamini na hasa kutumia uhuru walio nao wa kuchagua na kufanya maamuzi mbalimbali kwa ajili ya biashara zao. Unaweza kusema utafanya kila kitu kwa mafanikio, na mara nyingine pasipo kusikiliza maoni na ushauri wa watu wengine, hatimaye ukashindwa kutimiza mahitaji ya wateja wako. Badilisha fikra zako kisha ufanye mambo yako kwa kuzingatia maoni ya watu wengine kwani wao ndio wateja wako, na pengine wanaweza wakawa wanafahamu mengi zaidi kuhusiana na matakwa ya wateja kuliko unavyodhani. Kama matakwa haya yatatoka kwao, ni dhahiri kuwa biashara yako itakuwa inatimiza, kwa asilimia kubwa, mahitaji ya wateja na hivyo kuwafanya wasiende kununua bidhaa kwa washindani wako.
  Watenganishe Wateja Wazuri na Wale Wasumbufu
  Una haki na wajibu wa kuamua ni aina gani ya wateja ambao biashara yako itakuwa inawalenga. Andaa vigezo vya kuwafahamu wateja wasumbufu ili uweze kuwatenga na wale wazuri. Fanya zoezi hili mapema ili usije ukapoteza muda mwingi, pesa na jitihada nyingi katika kuwashawishi wateja ambao hawana mpango, wala hawawezi kufikiria kununua katika biashara yako, licha ya kulalamika kila mara wapunguziwe bei, huku wakitaka uwauzie bidhaa au huduma zenye ubora. Unatakiwa kufahamu vigezo utakavyoangalia kwa wateja watarajiwa. Vigezo hivyo ni pamoja na kuangalia gharama zinazotumika kumpata mteja, gharama za kumhudumia mteja au mteja wa kuhamahama. Aidha inapasa uwafahamu vyema wateja wasumbufu kwenye ulipaji, ambao pia mara nyingine si waaminifu. Mara nyingi wauzaji wanashindwa kuwatambua wateja wa aina hii mapema, na wanapowatambua, inakuwa ni vigumu kuwaondoa. Si rahisi kumfukuza mteja, ila jambo la msingi la kufanya ni kuwatambua walio muhimu sana katika biashara yako, ambao wakiondoka biashara itayumba. Tumia kila mbinu kuhakikisha huwapotezi wateja wa aina hii kwani tafiti zinaonesha kuwa wanafikia asilimia ishirini ya wateja wote, na wanachangia asilimia themanini ya mauzo yote ya biashara. Unaweza kupitia orodha ya wateja kwa kutumia mfano wa maswali yafuatayo:
  • Je, huyu ni mteja anayenipa faida? Ndiyo au Hapana
  • Je, huyu ni mmojawapo wa wateja ninaowalenga? Ndiyo au Hapana
  • Je, huyu ni mteja anayenunua sana bidhaa au huduma yangu?
  • Ndiyo au Hapana
  Mteja akipata “Ndiyo” tatu basi huyo ni mteja mzuri. Hata hivyo kama mteja akiwa na “Hapana” katika swali la kwanza na kufuatiwa na “Ndiyo” kwa maswali mawili yaliyobakia, huyo siyo mteja mzuri kwako kwa sasa. Jitahidi kumfanya alete faida katika biashara yako, au mwache moja kwa moja.
  Kujua mteja anafaidishaje biashara zingatia yafuatayo: fikiria ni wastani wa manunuzi ya shilingi ngapi anakupatia; ananunua bidhaa au huduma kila baada ya muda gani; kiasi cha faida kinachopatikana kila anapokuja kununua; jinsi anavyoweza kubadilika kuendana na mabadiliko ya bei; gharama zinazotumika kumhudumia; anavoweza kulipa kwa wakati bila kuchelewesha na pia ni watu wangapi wanaokuja kununua kwenye biashara kwa sababu wameelekezwa naye. Weka vigezo kulingana na aina ya biashara unayofanya.

  Tambua thamani ya wateja wako
  Unaweza ukawa umeelekeza nguvu zako zote katika kutafuta wateja wapya na kusahau thamani ya wateja waliopo katika biashara yako kwa sasa. Biashara yako inaweza isiendelee vizuri na kupata mafanikio endapo utawapoteza wateja wako wa kudumu. Kumbuka wateja hawa ndio utajiri na fursa kwako. Wanakuwa mara kwa mara wanakupa mawazo ya kuboresha zaidi, wanawaelekeza wengine kuja kununua katika biashara yako, gharama ndogo inatumika kuwahudumia na kama wakiondoka katika biashara itatetereka. Mteja mmoja ambaye hajaridhika na huduma katika biashara yako anaweza kulalamika kwa watu kati ya 6 hadi 10.Hakikisha unaweka mahusiano mazuri na wateja wako wa kudumu na ujifunze mengi kutoka kwao.
  Tafuta utofauti wa pekee
  Tafuta kitu ambacho kitakutambulisha kwa biashara yako na kukuweka juu ya washindani wako. Wateja wengi wanalinganisha bidhaa au huduma kabla hawajafanya maamuzi ya kununua. Wanatafuta sababu nzuri itakayowafanya wanunue kutoka katika biashara yako na wala si kwingine. Utapata wateja wengi endapo utafanya jitihada za kuwafahamu washindani wako. Hakikisha unatoa huduma ambayo ni bora zaidi kuliko ya washindani wako. Dunia ya sasa imekuwa ni ya ushindani katika kila nyanja.
  Zingatia hisia za wateja
  Hisia zinahusika sana katika kutoa uamuzi kuhusu kupenda, kununua na kutumia bidhaa fulani. Mchakato mzima wa uamuzi wa ununuzi hunaongozwa na hisia. Ili uweze kufanikiwa kushawishi ukubwa wa biadhaa au huduma zako kukubalika na wateja watarajiwa ni muhimu sana kulengesha matangazo yako katika kuamsha hisia za uhitaji zaidi kuliko kuweka nguvu nyingi katika punguzo la bei. Siyo kweli kwamba kila unapotoa punguzo la bei wateja watanunua bidhaa au huduma za biashara yako kwa wingi. Wakati wa kuandaa matangazo ni lazima uelewe na uhisi vitu ambavyo wateja wako walengwa wanavithamini katika kufanya umuzi ya uunuzi. Kwa upande mwingine, angalia pia ni jinsi gani wateja watarajiwa watakavyochukulia bidhaa au huduma za biashara yako. Mipango yote ya masoko, kwa ujumla, inatakiwa izingatie mambo ya msingi yanayogusa hisia zinazoleta mvuto kwa bidhaa au huduma zako, ili uweze kudumu na wateja wanaoiletea faida biashara yako.
  Wafanyabiashara wenye mafanikio ni wale wanaoweza kuzalisha bidhaa au huduma na kuzifikisha kwa wateja walengwa huku wakielewa na kuzingatia hisia za wateja, na kuwaacha wateja wamalizie mchakato huo kwa kulipa bei ambayo bidhaa au huduma husika imepangiwa.
  Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri ila kama utakosea katika kuandaa masoko, basi hutaweza kufikia mafanikio unayoyatamani. Anza kwanza kuzingatia jambo moja, “Masoko,” kisha utaona mabadiliko na utafanikiwa katika nyanja nyingine za biashara yako. Tukutane tena katika toleo lijalo ambapo nitawapa njia muhimu za kuandaa matangazo yenye tija kwa biashara yako, hasa kwa kutumia sayansi na teknolojia.

You must be logged in to reply to this topic.