• Author
  Posts
 • #814

  Mabula Emmanuel
  Keymaster

  Na Deodat Bernard
  +255 717 222 680

  Katika toleo lililopita uliweza kujifunza nini maana ya mtaji wa biashara, aina za mitaji na umuhimu wake wakati wa kuanza biashara. Katika makala haya utapata fursa ya kujifunza ukuzaji wa biashara na jinsi ya kupata mtaji kwa ajili ya upanuzi na uendelezaji wa biashara.

  Kwa kawaida ukuaji wa biashara unaweza kugawanywa katika hatua kuu nne: biashara inayoanza, inayokua, iliyokamaa au kuimarika na biashara iliyo katika hatua ya kudidimia. Mara nyingi biashara ambazo zinakua huwa na uhitaji wa pesa ya ziada wakati zikitaka kukua zaidi au kupanuka. Kupata pesa kwa ajili ya upanuzi wa biashara kunaweza kuwa na changamoto kubwa kama hakuna mpango madhubuti uliowekwa, au maandalizi mazuri.

  Kukuza na kupanua biashara ni jambo linalohitajika kufanywa kwa uangalifu na kuwekewa mipango madhubuti. Upanuzi wa biashara siyo jambo la kukurupuka tu. Huwezi kuamka asubuhi na kwenda kufungua tawi jingine kwa ajili biashara yako au kuanza kutengeneza bidhaa mpya! Uamuzi ya kupanua biashara lazima utokane na majadiliano yaliyofikiriwa kwa kina, huku mambo muhimu ya ukuaji wake yakizingatiwa. Mambo yanayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na utayari wa biashara kupanuka, utayari wa fedha na uwekezaji, miundombinu ya jinsi bidhaa zitakavyosafirishwa na kuwafikia walengwa na utayari binafsi wa wamiliki na rasilimali watu. Kanuni ni kuwa, unatakiwa kupanua biashara endapo tu umeshafanya utafiti na kuona kuna fursa ambazo hazijafanyiwa kazi, na ikiwa utazishughulikia zitainufaisha biashara yako. Inawezekana upanuzi wako ukalenga kundi fulani la watu katika jamii, au pengine kuna maeneo ambayo huduma za kibiashara hazijafikiwa hata na washindani wako. Upanuzi wa biashara haumaanishi kupata faida ya papo kwa hapo. Inaweza kuchukua muda mrefu zaidi endapo matumizi yatokanayo na upanuzi wa biashara yatakuwa makubwa ukilinganisha na ufanisi.

  Biashara hukua kwa namna mbili. Ukuaji wa ndani: Hili ni ongezeko katika nyanja zifuatazo ; uzalishaji, wafanyakazi, ujuzi, mauzo katika masoko au wateja. Ukuaji wa nje: Hii ni hali ya kuwa na huduma mpya au bidhaa mpya katika masoko uliyokuwa unahudumia mwanzo, au kuwa na bidhaa mpya katika masoko mapya, au bidhaa zilezile katika masoko mengine ambayo hukuwa unayafikia hapo awali.
  Katika ukuaji, biashara itahitaji mtaji-fedha ili kuweza kutimiza mahitaji yake ya ukuaji. Kwa kawaida, biashara ikishaanza, na kutimiza zaidi ya mwaka mmoja, na ikiwa inafanikiwa, inakuwa si vigumu kupatikana. Faida inayotokana na biashara mara nyingi hurudishwa kwenye biashara kwa dhamira ya ukuaji. Wawekezaji wengine huvutiwa na biashara kiasi kwamba huwa tayari kuwekeza fedha zao ili ziwe sehemu ya biashara husika. Hata hivyo watoaji wa mikopo wanakuwa wepesi wa kutoa fedha kwa biashara zinazokua na kupanuka. Kuna aina kuu mbili za mitaji- fedha inayoweza kupatikana wakati unapotaka kupanua biashara yako. Aina hizi za mitaji-fedha zinajumuisha:

  Akiba
  Sehemu ya utajiri unaotokana na uwekezaji na mafanikio ya biashara iliyofanywa siku zilizopita. Ili kujua thamani ya biashara yako, toa madeni yote kutoka katika rasilimali zilizopo kwenye biashara yako. Kuna biashara nyingine zinaendeshwa kwa kutumia pesa zinazotokana na faida ya biashara pekee. Pia endapo biashara itahitaji kiasi kikubwa cha fedha kama zinazohitajika wakati wa upanuzi, wamiliki wake huwekeza pesa kwenye biashara. Pia wapo wawekezaji watakaotaka kuweka pesa katika biashara na kuwa sehemu ya umiliki. Ingawa hii ni njia ambayo wafanyabiashara wengi hupenda kuitumia kwa ajilli ya upanuzi, inaweza kuwa ni ya gharama zaidi kiasi kwamba itahitaji maandalizi ya kuweka akiba kwa muda mrefu ili kukuza biashara.

  Mkopo
  Aina nyingine ya kupata pesa kwa ajili ya kukuza mtaji wa upanuzi wa biashara ni kwa kuchukua mkopo. Aina hii ya kukuza mtaji ni ya muda tu kwani kiasi cha pesa kilichoingia kwenye biashara kitaanza kupungua baada ya biashara kuanza kulipa mkopo. Biashara itakuwa inalipa mkopo na riba kwa kipindi wakopaji walichokubaliana na watoaji wa mkopo (Benki au vyanzo vingine vya mikopo). Kwa biashara zinazokua na ambazo hazijaimarika kiasi cha kuwa na utajiri mkubwa unaotokana na malimbikizo ya sehemu ya faida ya biashara, mkopo unaweza kuwa ni njia iliyo rahisi na ya haraka kwa ajili ya uwekezaji na upanuzi wa biashara.
  Ni lazima kupima na kufanya tathmini ili uone kama ukichukua mkopo utapata manufaa kwenye biashara yako. Faida ya wenye biashara itakuwa ni kiasi kilichosalia baada ya kulipa deni, ikijumuisha na riba ya mkopo. Kwa mfano kampuni ya DOBEA GROUP LTD ilikuwa na mpango wa kupanua biashara kwa kuanzisha tawi jipya katika jiji la Mbeya. Wamiliki wa DOBEA wakafanya uamuzi ya kuchukua mkopo kutoka benki ya biashara. Mkopo ulikuwa na thamani ya shilingi 10,000,000, ukiwa na riba ya 15%. Mkopo ulitakiwa kulipwa ndani ya miaka miwili. Baada ya kuufanyia kazi mkopo, kampuni ilipata jumla ya shilingi 18,000,000. Jumla ya riba iliyolipwa ni shilingi 1,500,000. Ili kujua faida iliyopatikana katika matumizi ya mkopo, unachukua kiasi cha riba na kujumlisha mkopo, jumla yake ni shilingi 11,500,000. Ukiitoa kwenye jumla ya pesa iliyopatikana utapata shilingi 6,500,000. Hii ndiyo faida iliyopatikana ambayo ni manufaa kwa kampuni. Faida hii isingekuwapo kama kampuni isingefanya uamuzi wa kuchukua mkopo.

  Mara nyingi kampuni zinazoamua kuongeza mtaji wa kukuza biashara zinafanya hivyo kwa lengo la kufanya mabadiliko makubwa kwenye biashara. Hizi ni kampuni ambazo zimeshakuwa kwenye nyanja za biashara husika kwa muda fulani wa kutosha na biashara inakuwa imeshapata uzoefu wa kutosha kuweza kustahimili misukosuko ya ndani na nje. Uzoefu unaonyesha kuwa kampuni zinazoamua kupanuka hufanya biashara kwa faida. Hata hivyo malimbikizo ya faida hayatoshi katika upanuzi mkubwa wa biashara, kuanzisha biashara mpya, kununua mashine au vifaa vya thamani kubwa au kuwekeza kwenye uzalishaji, matangazo na usambazaji wa bidhaa mpya.
  Kukodisha kwa mkataba (Leasing)
  Njia nyingine inayoweza kutumiwa na wafanyabiashara wakati wa upanuzi wa biashara ni kwa kutumia “leasing finance”. Hii inafanyika kwa makubaliano maalumu kati ya kampuni au taasisi ya kifedha inayotoa huduma ya kukodisha “leasing” kwa biashara inayotaka kutumia vifaa husika. Katika makubaliano mengine kunaweza kukawa na maamuzi kuwa mtumiaji atanunua na kumiliki mashine au vifaa vilivyopo kwenye makubaliano ya kukodisha ”leasing.” Au pengine makubaliano yanaweza kuwa baada ya muda wa leasing kwisha, vifaa vitarudishwa kwa mmiliki wa vifaa au mashine hizo. Njia hii hutumika ili kupata nyenzo kwa ajili ya kuwezesha upanuzi na ukuaji wa biashara na si kupata mtaji-fedha

  Hadi kufikia hapo, umepata kufahamu ni wakati gani upanue biashara yako na ni aina gani ya mitaji ambayo unaweza kuitumia kwa ajili ya upanuzi na ukuaji wa biashara. Usikose toleo lijalo ambapo utajulishwa ni kwa nini uweke akiba kwa ajili ya kuboresha mtaji wa biashara.

You must be logged in to reply to this topic.