• Author
  Posts
 • #816

  Mabula Emmanuel
  Keymaster

  Elimu ya Uwekezaji
  Na Douglas Damas

  Katika makala iliyopita tulipata fursa ya kujifunza maana ya uwekezaji,nani hasa anayetambuliwa kama mwekezaji,aina ya vitega uchumi na umuhimu wake.Katika makala haya tutajifunza kwa kina uwekezaji kwenye hisa,lengo likiwa kukupatia msingi unaohitaji kwa ajili ya kufanya maamuzi yako binafsi ya uwekezaji.Tutaanza na kujifunza nini maana ya hisa,aina za hisa,na halafu tutazungumzia ni jinsi gani hisa zinanunuliwa na kuuzwa,nini kinasababisha bei kubadilika,faida na hatari ya kuwekeza kwenye hisa n.k.
  kwa watu tofauti.Hii inamaanisha kuwa watu tofauti wanawekeza kwenye vitu tofauti,kwasababu watu tofauti wanahitaji vitu tofauti.Kwa mfano baadhi ya watu wanawekeza kwenye kuwa na familia kubwa.Familia kubwa kwa watu wengine ni njia ya kujihakikishia matunzo katika umri wao wa uzeeni.Watu wengine wanawekeza kwenye elimu nzuri,itakayokuwa na uhakika wa kazi na mafao.Baadhi ya watu wanawekeza kwenye vitega uchumi vya nje kama vile hisa,hatifungani,biashara,nyu mba za kupangisha,viwanja.vito vya thamani n.k.Katika marekani,takribani asilimia arobaini na tano(45%) ya watu wote wanamiliki hisa katika makampuni.Idadi hii inaongezeka kadiri watu wanavyotambua kwamba uhakika wa kazi na ajira ya kudumu zinapungua na katika uchumi huu mpya hakuna garantii tena ya matunzo wakati wa uzeeni kwa kuwa na watoto wengi.
  Bila shaka, ungelipenda kuwa mmiliki wa biashara bila kuhitajika kufanya kazi katika biashara husika.Hebu fikiri kama ungaliweza kufanya mambo mengine, ilhali ukishuhudia kampuni yako ikikua, na unapokea hundi za gawio la fedha kama sehemu ya faida inayoingia kwenye kampuni! Hali hii inaweza kuonekana kama ndoto, lakini inakaribiana na hali halisi kuliko unavyofikiria.

  “ Bila shaka, ungelipenda kuwa mmiliki wa biashara bila kuhitajika kufanya kazi katika biashara husika.Hebu fikiri kama ungaliweza kufanya mambo mengine, ilhali ukishuhudia kampuni yako ikikua, na unapokea hundi za gawio la fedha kama sehemu ya faida inayoingia kwenye kampuni!”

  Bila shaka umehisi kinachoongelewa hapa, tunaongelea suala la kumiliki hisa.Aina hii ya chombo cha kifedha kilichobuniwa,bila shaka ni moja ya zana kuu zilizogunduliwa kwa ajili ya kujenga utajiri.Hisa ni sehemu kama siyo jiwe la msingi,la karibia kila vitega uchumi vya uwekezaji.Unapoanza safari yako ya kutafuta uhuru wa kifedha,unapaswa kuwa na uelewa wa kina wa hisa na namna inavyouzwa na kununuliwa katika soko la hisa. Katika kipindi cha miongo michache iliyopita, hamu ya watu wa kawaida duniani kuingia katika masoko ya hisa imeongezeka maradufu.Kile ambacho mwanzo kilionekana kama kitu cha matajiri sasa kimegeuka kuwa chombo huru kwa ajili ya kujijengea utajiri.Uhitaji huu ukifungamanishwa na kukua kwa teknonolojia ya kufanya biashara umefungua masoko kiasi kwamba siku hizi karibia kila mtu anaweza kumiliki hisa. Licha ya umaarufu wake, hata hivyo, watu wengi hawaelewi hisa kwa ukamilifu.Wengi wanajifunza kutoka kwa watu wengine ambao nao pia hawafahamu ni nini wanachozungumza. Bila shaka umekwisha kuwasikia watu wakisema vitu kama,“Jamin amepata faida kubwa baada ya kuuza hisa zake katika kampuni XYZ,na sasa amepata tetesi za hisa nzuri katika kampuni UVW ” au “Chunga sana uwekezaji kwenye hisa—unaweza kupoteza kila kitu katika kipindi cha siku kadhaa tu!” Nyingi ya hizi taarifa potofu zinatokana na mtazamo wa watu kutaka kupata fedha haraka haraka,ulioshika hatamu kipindi cha soko la dotcom huko Marekani mwishoni mwa miaka 1990.Watu walifikiri kuwa hisa zilikuwa majibu ya kupata utajiri wa haraka usio kuwa na hatari.Kuanguka kwa soko la dotcom kulithibitisha kuwa hisa ziliambatana na hatari.Hisa zinaweza na zinazalisha kiasi kikubwa cha utajiri,lakini zinaambatana na hatari pia.Suluhisho ni moja tu nalo ni elimu.Ngao ya kukulinda katika soko la hisa ni kuelewa ni wapi unaziweka fedha zako.

  “Hisa zinaweza na zinazalisha kiasi kikubwa cha utajiri, lakini zinaambatana na hatari pia.Suluhisho ni moja tu nalo ni elimu.Ngao ya kukulinda katika soko la hisa ni kuelewa ni wapi unaziweka fedha zako”.

  HISA NI NINI?
  Katika maana rahisi na ya wazi, hisa ni sehemu ya rasilimali za kampuni.Hisa zinawakilisha kiasi cha udhibiti wako katika rasilimali/aseti na mapato ya kampuni.Kadiri unavyonunua hisa nyingi zaidi, sehemu ya umiliki wako katika kampuni husika unaongezeka.Aidha ukisema hisa, equiti au stoku, vyote vinamaanisha kitu kimoja.
  Kuwa mmiliki.
  Kama una hisa katika kampuni inamaanisha kwamba wewe ni mmoja wa wamiliki wengi wa kampuni husika (wanahisa) na hivyo una haki ya kila kitu kampuni inamiliki. Ndiyo,hii inamaanisha kwamba kimsingi unamiliki sehemu ya fenicha,nyumba,kila nembo ya biashara na kila mkataba kampuni inashikilia n.k.Kama mmiliki,una mamlaka na sehemu ya mapato ya kampuni sambamba na haki ya kupiga kura inayoambatana na hisa unazomiliki.
  Hati ya Hisa.
  Hisa inawakilishwa na hati ya hisa.Hiki ni kipande cha karatasi kilichobuniwa na kutolewa na kampuni kisheria ambacho ni ushahidi kwamba unamiliki hisa katika kampuni husika. Katika zama hizi za kompyuta na intaneti,hakika unaweza kutoziona nyaraka hizi kwasababu dalali wako anahifadhi kumbukumbu zako katika mfumo wa kieletroniki.Mfumo wa kieletroniki unatumika kuzifanya hisa zako kununulika na kuuzika kirahisi.Katika kipindi cha nyuma,wakati mtu akihitaji kuuza hisa zake,mtu huyu alipaswa kuchukua hati yake kwenda kwa dalali.Lakini sasa katika nchi nyingi biashara inafanywa kwa kompyuta,intaneti na kupiga simu na kufanya maisha kuwa rahisi kwa kila mtu.

  Taarifa muhimu zilizopo katika hati ya hisa ni kama ifuatavyo;Namba ya hati,aina ya hisa unazomiliki,idadi ya hisa unazomiliki,jina la kampuni,namba ya kampuni,jina kamili la mwanahisa,anuani ya makazi ya mwanahisa,thamani ya hisa unazomiliki,jina&sahihi ya mkurugenzi wa kampuni anayeidhinisha,jina&sahihi ya katibu wa kampuni anayeidhinisha
  Kwa kuwa mwanahisa wa kampuni la umma haimaanishi kuwa una uwezo wa kuingilia shughuli za kuendesha biashara, badala yake, una mamlaka ya kura moja kwa kila hisa unayomiliki kwa ajili ya kuchagua bodi ya wakurugenzi wakati wa mikutano ya kufunga mwaka.Huo ndio ukomo wa usemaji wako katika kampuni.Kwa mfano,kwa kuwa mwanahisa wa Precious air haimaanishi kwamba unaweza kumpigia Shirima na kumwelekeza au kumwamrisha ni jinsi gani unafikiri anaweza kuiongoza kampuni hiyo. Menejimenti ya kampuni inapaswa kuongeza thamani ya kampuni kwa ajili ya wanahisa wake.Kama hili halitatokea, wanahisa wanaweza kupiga kura kuiondoa menejimenti iliyopo (kinatharia).Katika hali halisi utakuta wawekezaji binafsi kama wewe na mimi hatuna hisa za kutosha kuleta ushawishi katika kampuni.Kihalisia ni wale tu wenye hisa nyingi katika kampuni ndio wanaweza kufanya maamuzi. Kwa wanahisa wa kawaida,kutokuwa na uwezo wa kusimamia na kuendesha kampuni siyo jambo la kusumbukia,kwasababu,dhumuni ni kwamba hauhitaji kulazimika kufanya kazi kwa ajili ya fedha,fedha inakufanyia kazi.Umuhimu wa wewe kuwa mwanahisa ni kwamba unakuwa na mamlaka na sehemu ya faida ya kampuni na kuwa na haki na udhibiti wa sehemu ya rasilimali za kampuni husika.Faida inalipwa katika mfumo wa gawio.Kwa kadiri unavyomiliki hisa nyingi,ndivyo hivyo unavyopata sehemu kubwa ya faida ya kampuni.Stahili zako juu ya mali/aseti za kampuni utazipata pale unapoamua kuuza hisa zako.Kampuni inapofilisika mali zake zitauzwa,basi utapokea mgawo unaosalia baada ya watu waliyoikopesha kampuni(wadeni) wote kumalizika kulipwa.

  “Umuhimu wa kumiliki hisa kwenye kampuni ni kuwa na haki juu ya aseti/mali na mapato ya kampuni”.
  Kwanini Kampuni zinauza hisa zake?
  Kwanini waanzilishi wa kampuni wanagawana faida na maelfu ya watu wengine wakati wao wenyewe wangeliweza kuitumia wenyewe? Sababu ni kwamba katika wakati fulani kila kampuni inahitaji kuongeza mtaji. Kufanya hivyo,kampuni zinaweza aidha kukopa kutoka kwa taasisi za fedha au kuongeza mtaji kupitia kuuza sehemu ya kampuni,ambayo inajulikana kama kuuza hisa.Kuuza hisa ina faida kwa kampuni kwa sababu kampuni haihitajiki kurejesha fedha au kulipa riba.Wanahisa wanachokipata kama mrejesho ni matumaini kwamba siku moja hisa zao zitakuwa na thamani zaidi ya kile walicholipia awali. Mauzo ya kwanza ya hisa,yanayotolewa na kampuni binafsi,yanaitwa toleo la mwanzo kwa umma (IPO).
  Hatari na faida zinazoambatana na uwekezaji kwenye hisa.
  la hisa zako.Baadhi ya makampuni yanatoa gawio, gawio ni fedha taslimu wanayopewa wanahisa kama sehemu ya faida iliyozalishwa na kampuni kufikia mwisho wa kila mwaka wa fedha.Kuna makampuni yenye sera ya kutoa gawio kila mwaka mwa wanahisa wake, ni vema kuongea na mshauri wako wa masuala ya kifedha aweze kukuambia baadhi ya makampuni haya.lakini makampuni mengi hayatoi gawio. Na hata hivyo makampuni hayalazimiki kutoa gawio. Bila kupewa gawio,mwekezaji anaweza kupata faida kutokana na kuongezeka kwa thamani ya hisa zake katika soko la hisa na hivyo kuweza kuamua kuuza sehemu ya hisa zake.Lakini kwa upande mwingine,hisa yoyote inaweza kupoteza thamani yake yote na katika hali hiyo uwekezaji wako unakuwa hauna thamani yeyote.Ijapokuwa hatari inaonekana kuwa kubwa,kuna upande mwingine wenye matumaini pia.Kuthubutu kuchukua hatari kubwa inamaanisha marejesho(ritani) ya uwekezaji wako kuwa kubwa.Hii ndiyo sababu inayojibu swali la kwanini hisa katika historia zimekuwa zikizidi vitega uchumi vingine kama hatifungani na akaunti za akiba,hii ni kutokana na sababu kuwa mfumuko wa bei upo juu zaidi kuliko kiwango cha riba kinachotolewa na mabenki ya biashara.Kiwango cha ukuaji wa hisa ni maradufu zaidi kuliko viwango vya riba vya benki.Katika kipindi cha muda mrefu,uwekezaji katika hisa umekuwa na historia ya kuwa na ritani ya asilimia 10 -12%.

  Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na mahitaji makubwa ya hisa za kampuni ya simenti ya Benue ya nchini Nigeria ambapo wakati wa awali hisa moja ilikuwa ikichuuzwa kwa naira 6 kwa hisa.Kutokana na kuadimika kwake na kufanya vizuri kwa kampuni hiyo,hisa moja kwa sasa inachuuzwa kwa takriban naira 48 kwa hisa. Hii inamaanisha kuwa kulikuwa na ongezeko la asilimia 700 katika thamani ya hisa.Kama ulikuwa umenunua hisa 50, 000 wakati zikiuzwa naira 6 kwa hisa,ukiwa umetumia naira 300,0000 kuzinunua hisa hizo.Sasa,hisa moja ikiwa inagharimu naira 48 kwa hisa,ukiamua kuuza hisa hizo,mapato yako yangelikuwa 48×50,000,ambayo ni sawa na naira milioni 2.4.Kwa hiyo mtaji wako uliouwekeza kwenye kampuni hii umeongezeka kutoka naira 300,000 mpaka naira milioni 2.4.Kwa kweli biashara ya hisa ina uwezo wa kukufanya kuwa milionea ndani ya usiku mmoja tu.
  Aina za Hisa.
  Hisa zimegawanyika katika aina kuu mbili ambazo ni: Hisa za kawaida (ordinary shares) na Hisa maalum(prefered shares), hata hivyo kuna aina nyingine za hisa kama hisa zenye warantii, hisa huru n.k.
  “Hisa zimegawanyika katika aina kuu mbili ambazo ni: Hisa za kawaida (ordinary shares) na Hisa maalum (prefered shares), hata hivyo kuna aina nyingine za hisa kama Hisa zenye warantii, Hisa huru n.k”
  Hisa za kawaida.
  Watu wanapozungumzia hisa mara nyingi wanamaanisha aina hii ya hisa.Hisa za kawaida zinawakilisha umiliki katika kampuni na stahili ya kupata gawio kutokana na faida inayotengenezwa na kampuni.Mwekezaji anapata haki ya kura moja kwa kila hisa anayomiliki kwa ajili ya kuchagua wajumbe wa bodi,ambao ndio wenye wajibu wa kufuatilia maamuzi muhimu yanayofanywa na menejimenti ya kampuni.

  Katika kipindi cha muda mrefu, hisa za kawaida kwa njia ya ongezeko la mtaji,zinatoa ritani kubwa kuliko takriban kila kitega uchumi kingine.Ritani hii kubwa inakuja kutokana na ukweli kwamba hisa za kawaida zimebeba hatari kubwa zaidi.Kama kampuni itafilisika na mali zake kuuzwa,wanahisa wa kawaida hawatapokea fedha mpaka wadai wote,wamiliki hatifungani wote na wamiliki wa hisa maalum wote watakapolipwa.
  Hisa maalum/hisa za kipaumbele.
  Wamiliki wa hisa maalum ndio wanaopewa kipaumbele katika kununua hisa kabla ya wengine. Ni kategori ya umiliki wa hisa katika kampuni ambapo mmiliki wa hisa maalum ana mamlaka makubwa kwenye aseti/mali na mapato ya kampuni kuliko ilivyo kwa mmiliki wa hisa za kawaida,hii ni kutokana na ukweli kwamba kampuni inapofilisika wamiliki wa hisa maalum ndio wanaolipwa kwanza.Mmiliki wa hisa maalum ni lazima alipwe gawio lake kwanza kabla ya gawio halijatolewa kwa wamiliki wa hisa za kawaida.Hata hivyo mmiliki wa hisa maalum hana haki ya kupiga kura ya kuchagua wajumbe wa bodi.
  Ukitaka kupata taarifa za kina kuhusiana na muundo wa aina hii ya hisa, tembelea kampuni ambayo ungependelea

You must be logged in to reply to this topic.