• Author
  Posts
 • #811

  Mabula Emmanuel
  Keymaster

  Katika makala haya tunakuletea uchambuzi kuhusu mjasiriamali anayechipukia Tanzania. Uchambuzi huu utajumuisha historia yake kimaisha; kiwango chake kielimu; tabia binafsi; maadili; kanuni na nidhamu aliyonayo; kipato chake; biashara au teknolojia alizoibua; mahusiano na maisha yake kifamilia. Aidha tutajifunza namna anavyoendesha biashara; namna anavyokabiliana na changamoto mbalimbali, mawazo, maoni na ushauri wake hasa kwa vijana wanaoingia katika ujasiriamali.
  Katika toleo hili, tunakuletea mjasiriamali mwanamke anayechipukia Tanzania, ambaye ni Emelda Mwamanga Mtunga, Mkurugenzi na Mwenyekiti wa kampuni ya RELIM Entertainment Ltd. Emelda Mwamanga Mtunga alizaliwa mnamo tarehe 21 mwezi wa nne mwaka 1979, katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es salaam.Baba yake anaitwa Izack Mwamanga akiwa ni mfanya biashara. Anaendesha kampuni ya magunia inayoitwa Tanzania Bag Corporation Ltd (TBC (1998) Ltd pamoja na kumiliki kampuni ya kutengeneza maji ya chupa yanayoitwa Umoja.. Mama yake Lydia George Mwamanga ambae ni mwalimu Mstaafu wa shule ya msingi Oysterbay – Dar es salaam. Emelda ameolewa na Baraka Mtunga, ambaye ni mhandisi Katika tasnia ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT). Alipotimiza umri wa miaka saba, alianza kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Oysterbay, kisha akaendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Jangwani. Baadaye alichaguliwa kuendelea na masomo ya PCB katika ngazi ya A-level, lakini yeye hakupendelea sana masomo ya sayansi hivyo aliamua kuchukua masomo ya HGL, katika Shule ya Sekondari,Shaaban Robert High School, Dar es saalam. Emelda anasema uamuzi huo ulitokana na mjomba wake kuwa mwanasheria, hivyo alijikuta akipenda sana kusomea uanasheria. Vilevile wazazi wake walitamani sana awe mwanasheria kama mjomba wake. Anasema Mara nyingi baada ya masomo alikuwa akiwasadia wazazi wake shughuli ndogondogo na kujisomea
  Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Cape Town (UCT) nchini Afrika ya Kusini, hadi Desemba 2002 alipohitimu akiwa na shahada ya usimamizi wa rasilimali watu (HR). Mwaka 2003, baada ya kuhitimu masomo yake, alifanikiwa kupata ajira katika kampuni ya vinywaji ya Coca Cola, iliyoko Mikocheni jijini Dar es salaam, kama Ofisa wa Usimamizi Rasilimali Watu (HR Officer).Baadaye aliweza kuwa Meneja Rasilimali Watu wa kampuni ya Coca Cola kutokana na utendaji wake wa kazi kuwa mzuri. Anasema alipata usimamizi na mwongozo mzuri katika suala zima la uongozi kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi wake, Caroline Temu Kavishe. Uzoefu huu ulimsaidia sana alipoanzisha kampuni yake kwani ulimpatia uwezo na upeo mkubwa wa kusimamia na kuongoza wenzake.
  Akiwa anasoma nchini Afrika ya Kusini, aliweza kuona majarida tofauti tofauti ya mitindo katika supermarket na maduka mbalimbali nchini humo.Pia kampuni ya Coca Cola ilikuwa na jarida ambalo lilichapishwa nchini

  Afrika ya Kusini. Jarida hilo liliongelea masuala ya kampuni na wafanyakazi wa Kampuni ya Coca Cola. Kwa vile Emelda alipewa nafasi ya kuandaa jarida hilo aliwahoji wafanyakazi katika kampuni, wakiwemo wakurugenzi na mameneja. Anasema jarida lilipotoka, wafanyakazi walivutiwa sana na kazi yake. Hali hiyo ilimhamasisha na akaona uwezekano wa kuanzisha jarida lake mwenyewe aliloliita Bang. Jina Bang linamaanisha, ‘amini pasipo kukata tamaa’ (Believe And Never Give Up). Jarida hili linaongelea masuala ya mitindo (fashion). Fursa aliyoiona katika tasnia ya mitindo nchiniTanzania, ndiyo iliyomhamasisha kuanzisha jarida hilo.
  Mnamo mwaka 2004 ndipo shughuli rasmi za kuandaa jarida la Bang zilipoanza.Emelda anasema alipewa ofisi ndogo katika kampuni ya baba yake. Baadaye alisajili kampuni yake ya RELIM Entertainment Ltd kwa ajili ya kufanya shughuli za jarida. Anasema jina RELIM ni vifupisho vya majina ya familia. Hadi kufikia mwaka 2005, aliweza kuchapisha toleo lake la kwanza, kwa kuanza na nakala 5,000. Jarida hili alilichapisha bila ya matangazo ya kulipia. Hivyo basi, matangazo yaliyokuwapo aliyatoa bure ili aweze kuuza nakala atakazochapisha. Alipata mtaji wa kufanyia uchapishaji wa jarida kutokana na mkopo pamoja na mshahara wake aliokuwa akidunduliza. Wakati huo alijikuta akifanya kazi hadi usiku sana; alifanya kazi mchana katika kampuni ya Coca Cola, na jioni aliandaa jarida la Bang katika ofisi ndogo aliyopewa na baba yake.
  Kama tulivyoona katika toleo la kwanza, hakuweza kuuza matangazo kwa vile jarida lao lilikuwa bado geni katika soko. Isitoshe, kutokana na ugeni wa jarida hili, uuzaji wa nakala walizochapisha nao ulikuwa mgumu. Alijikuta katika hasara kubwa. Anasema alijisikia kulia kutokana na hasara aliyopata kwani mshahara aliodunduliza na mkopo aliochukua-vyote vilipotea! Hata hivyo anamshukuru Mungu maana alipata msaada wa hali ya juu kutoka kwa wazazi wake. Anasema baba yake alimfadhili fedha ambayo ilimuwezesha kuchapisha toleo la pili.
  Mnamo mwaka 2005 Mei, baada ya kufanya kazi kwa kipindi cha miaka miwili katika kampuni ya Coca Cola, aliamua kuachana na kazi ya kuajiriwa ili aweze kuelekeza nguvu na muda mwingi katika kampuni yake ya RELIM, hasa katika kusambaza na kuuza majarida. Aliona atumie muda mwingi katika kampuni yake ili ahakikishe inasimama. Alisaidiana na mbia wake, Caroline Daftari, ambaye alikuwa muhitimu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW). Caroline naye alikuwa kaajiriwa lakini aliacha kazi ili kuiimarisha kampuni yao ya RELIM.Yeye pamoja na washirika wengine walikuwa na hamasa kubwa ya kuhakikisha biashara yao inakua.
  Baada ya toleo la pili, waliweza kuwa na ofisi yao ya kwanza huko Mbezi, jijini Dar es salaam. Kwa sasa ofisi za kampuni ya RELIM Entertainment Ltd zipo BANG House Mikocheni, jijini Dar es salaam. Emelda anasema kutokana na elimu pamoja na uzoefu aliopata katika kazi ya usimamizi wa rasilimali watu, ameweza kujenga timu imara ya wafanyakazi katika kampuni yake ya RELIM Entertainment Ltd. Anasema hivi sasa ana timu ambayo anaiogoza vizuri, hivyo hupata matokeo mazuri. Hata kama hayupo ofisini wafanyakazi wake huweza kutekeleza shughuli za kampuni bila matatizo. Hali hii inatokana na uongozi wake mzuri, ambao umemwezesha kujenga timu imara.
  Emelda anasema baada ya kuanzisha jarida ilimchukua miaka mitatu kurudisha gharama za uendeshaji wa kampuni. Aidha alianza kupata faida baada ya miaka 3, ambapo katika kipindi hicho, ndipo kampuni yake ya RELIM iliweza kuajiri wafanyakazi.
  Kwa sasa kampuni ya RELIM Entertainment Ltd pamoja na jarida lake la Bang lina miaka 9. Aidha wanauza majarida yao takribani katika nchi zote za Afrika ya Mashariki, kama vile Uganda, Kenya na Zambia. Hapo awali kampuni ya RELIM Entertainment Ltd iliweza kuuza nakala nyingi katika nchi hizi, lakini kampuni ya True Love ambayo waliingia nayo ubia wa kusambaza jarida la Bang nchini Kenya ilianza ukiritimba baada ya kuona jarida hili lina ushindani mkubwa. Kampuni ya True love nayo ilikuwa ikifanya uchapishaji wa majarida nchini Kenya. Kwake hii ilikuwa ni changamoto kubwa maana soko lake la nje lilielekea kufa. Hata hivyo aliweza kutatua tatizo hili baada ya kuingia katika mkataba mpya wa usambazaji na kwa sasa anauza nakala zake Afrika ya Mashariki, japo si kwa kiasi kikubwa kama ilivyokuwa awali. Mwaka 2009 aliweza kupata nafasi ya kwenda nchini Marekani kupeperusha bendera ya Bang na aliweza kukutana na mwanamama tajiri aliyekuwa mkurugenzi na mwenyekiti wa Time Inc aitwaye Anne Moore na chini ya huyu mama Emelda alipata kukutana na watu mashuhuri kama Oprah, Vijana wawili wamiliki wa Twitter, Whoopi Golberg, na wengine katika sherehe moja iliyo andaliwa na Time Inc. sherehe hii inaitwa ‘Time 100 party.” Ni sherehe inayo fanyika mara moja kwa mwaka katika jiji la Newyork na huwa inaalika watu mashuhuri 100 kwa kila mwaka, hivyo anasema aliweza kujifunza masuala mengi kuhusiana na biashara. Pia mwaka 2012 alipewa tuzo za TIAW ambazo zilitolewa nchini Marekani jijini Washington DC, pia Emelda ni mwanachama wa Global Aspen Leadership katika
  uongozi Africa.
  Kwa sasa Emelda ameolewa na ni mama wa mtoto mmoja anaitwa Gabrielle Anasema ingawa ameolewa, bado anapata ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa mumewe Baraka Mtunga. Anasema mumewe anaelewa yeye anafanya nini kwa hiyo anajitahidi kumsaidia kwa mawazo na mambo mengineyo kadha wa kadha, katika kuhakikisha kampuni yake ya RELIM Entertainment Ltd inafanikiwa.
  Emelda anasema changamoto katika biashara ni nyingi lakini kinachotakiwa ni kuwa imara katika kusimamia nia na malengo yako, ili kuhakikisha yanatimia pasipo kukata tamaa wala kurudi nyuma. Anasema, “angalia ni namna gani ya kutatua tatizo lako na kama unaona huwezi, ni vyema kuwatafuta wataalamu wa biashara wakusaidie ushauri na mawazo.” Anaendelea kusema makosa katika biashara ni sehemu ya kujifunza hivyo unapokosea usikate tamaa bali jisahihishe na kisha endelea mbele. Mara nyingi Emelda anapokumbana na changamoto hufunga na kumuomba Mungu amsaidie katika kutatua matatizo yake. Pia anasema suala zima la uongozi kwa wafanyakazi ni kitu ambacho kinafanya makampuni mengi kufa. Anashauri kwamba inampasa kiongozi wa biashara kusimamia vyema wale anaowaongoza, ili aweze kupata matokeo mazuri hata kama ikitokea hayupo katika eneo la kazi.
  Anatoa maoni na ushauri kwamba, kwa vileTanzania ni nchi inayokua kwa kasi kiuchumi, wawekezaji kutoka mataifa ya kigeni wanataka sana kuwekeza humu nchini. Anasema vijana ambao ndio taifa la leo, waangalie fursa zilizopo nchini mwetu na kuhakikisha wanazifanyia kazi. Pia serikali ijitahidi kuwapa msaada wanapoanzisha kitu ambacho kitawakomboa wao pamoja na taifa lao. Anasema mpango kama huo utasadia kwani wawekezaji wakija wataingia ubia na wazawa.Hali hiyo ikisimamiwa vyema, italeta uwiano katika suala zima la uwekezaji na uchumi. Anaendelea kusema kuwa, kama hautakuwepo uwiano katika kumiliki uchumi, basi taifa na watu wake litaingia katika utumwa wa kutumikia wawekezaji wa nje (wageni).
  Aidha anaendelea kusema kuwa katika kuanzisha biashara, ni vyema kuhakikisha unajitahidi kuwa mbunifu na kufanya vitu ambavyo ni tofauti na wenzako. Mtindo uliozoeleka wa kumwona mwenzako ana duka au baa na wewe unaanza kufanya biashara hiyohiyo pembeni mwake haufai. Anasema kwa njia hiyo, utakuwa wewe si mjasiriamali bali ni mfanyabiashara wa kawaida tu. Anasema siku zote mjasiriamali ni mbunifu; ni mtu ambaye anaziona fursa pamoja na kuzitumia. Anaendelea kusema vijana wasitegemee serikali katika kubadili maisha yao, bali wajiulize wanataka kulifanyia nini taifa na si taifa liwafanyie nini.
  Ndoto na mipango ya Emelda ni kuhakikisha kampuni yake ya RELIM Entertainment Ltd inakuwa na kufika mbali zaidi. Pia anataka jarida lake la Bang lifanikiwe kama jarida la Times Magazine. Awali kabla ya kuanzisha majarida, alipenda sana kuwa na kipindi katika televisheni kama alivyo Oprah. Hata hivyo hivi sasa yupo kwenye harakati za kuhakikisha anafanikisha lengo lake hilo.
  Katika toleo lijalo tutakuletea mjasiriamali mwingine anayechipukia nchini Tanzania; teknolojia na biashara aliyoibua ili kufanya maisha ya jamii yetu kuwa mazuri. Tutaweza kuona mazingira aliyokulia na mafanikio aliyo nayo sasa.

You must be logged in to reply to this topic.